Subscribe:

Saturday, 16 January 2016

SIKU YA 09:

       KRISTO AKIAKISIWA NDANI YA KANISA:
 
“Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi. (Yohana 17:23)


• Anzeni kipindi chenu cha maombi kwa kumsifu Mungu kwamba Yeye ni furaha, amani na uvumilivu n.k
• Mtukuze Mungu kwamba ameliita kanisa Lake la masalio kuwa nuru kwa ulimwengu.
• Mtukuze Mungu kwamba ataikamilisha kazi aliyoianzisha katika kanisa.
Kuungama na Kudai Ushindi dhidi ya dhambi (kama dakika 5)
• Muombe Mungu akuonyeshe dhambi unazohitaji kuziungama faraghani. Dai ushindi dhidi ya dhambi hizo.
• Muombe Mungu msamaha kwa nyakati ambazo uliruhusu wivu, kushuku au kutafuta makosa kwa ndugu zako ndani ya moyo wako. Omba kwa ajili ya moyo mpya ukijazwa na upendo pamoja na huruma.
Sala na Maombezi
• Muombe Mungu aandae moyo wako kumpokea Roho Mtakatifu.
• Omba kwa ajili ya familia yako ili iunganishwe na kwamba amani na upendo vitawale makanisa yetu.
• Omba ili Mungu atakase kanisa ili wageni wahisi uwepo wa Roho Mtakatifu.
• Omba ili viongozi wa kanisa (mchungaji wako wa mtaa, wachuganji wa konferensi, unioni, divisheni na Makao Makuu ya Kanisa) wafanye kazi kwa upendo, huruma na umoja katika kumaliza kazi waliyopatiwa na Kristo.
• Omba kwa ajili ya umoja kote ulimwenguni katika mikusanyiko ya kikanisa na upekee wa kanisa ukijengwa katika kuheshimu Neno la Mungu, maombi yenye unyenyekevu, nguvu ya Roho Mtakatifu, kuheshimu sera za kanisa zilizopitishwa na kujiingiza kikamilifu katika utume wa kanisa.
• Omba kwa ajili ya unyenyekevu katika maisha yetu ili tuweze kuunganishwa tunapojitoa katika kutii uongozi wa Mungu na mchakato wa kanisa katika kufanya maamuzi ambayo huamuliwa pamoja na kukubali mapendekezo yatakayopitishwa katika ngazi ya Makao Makuu ya Kanisa.
• Omba ili kwamba tuweze kutoa muda wetu zaidi katika mambo ya umiele kupitia kujifunza Biblia na maombi, ili kumruhusu Mungu kuongoza kwa ukamilifu watu wake kulingana na mapenzi Yake na sio mapenzi yetu. Hii itatusaidia kutuweka daima karibu na Mungu na kuruhusu nguvu ya Roho Mtakatifu kugeuza mazoea ya kiulimwengu ambayo huliweka matatani kanisa la Mungu na maisha yetu ya kila siku.
• Utume Katika Miji Mikuu – Omba kwa ajili ya divisheni yetu ya East –Central Africa na miji tuliyochagua kuifanyia kazi huko: Kinshasa, Dar-es-Salaam, Addis Ababa, Kampala, Kananga, Lodwar, Kigali, Lubumbashi, Goma, Magara na Juba. Omba ili ngome imara za shetani zivunjwe, mahusiano pamoja na Kristo yajengwe.
• Omba kwa ajili ya ulinzi kwa vijana na sisi sote kutoka katika mivuto inaoongezeka kila siku ya kidunia. Omba ili tuweze kuweka kipaumbele katika Neno la Mungu na huduma kwa wengine. Omba ili makanisa mahalia yaweze kudhamini vijana katika utume nje ya kanisa na fursa za kutoa huduma.
• Omba ili watu saba au zaidi katika orodha yako waone hitaji la kufungua mioyo yao kwa Roho Mtakatifu.
• Omba kwa ajili ya mahitaji binafsi uliyo nayo.
Shukrani (dakika 10)
• Mshukuru Mungu kwa kile alichofanya katika kanisa Lake na kile atakachokifanya katika kanisa.
• Mshukuru Mungu kwamba yuko tayari kusafisha, kutakasa na kuongoza kanisa.
• Mshukuru Mungu kwamba anafanya kazi katika mioyo ya wale ambao unawaombea.
Mapendekezo ya Nyimbo
Tutajenga juu ya Mwamba no. 72, Msingi wa Kanisa no. 195, Yote Namtolea Yesu no. 122,
KRISTO AKIAKISIWA NDANI YA KANISA
“Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi. Yohana 17:23
Hakuna kitu cho chote ambacho kinaweza kuhafifisha mvuto wa kanisa kama kukosekana kwa upendo….. Watu wa kidunia wanatuangalia ili kuona kile imani inachofanya katika tabia na maisha yetu. Wanaangalia kuona kama imani hiyo ina matokeo ya kuleta utakaso katika mioyo yetu, kama tumebadilishwa kufanana na Kristo. Wako makini kugundua kila dosari katika maisha yetu, kila kukosa msimamo katika matendo yetu, hebu tusiwape nafasi kukebehi imani yetu. Sio upinzani duniani ambao utatuweka hatarini bali ni uovu unaoendekezwa katikati yetu ambao huleta matokeo ya kutisha. Ni maisha ya watu wasiojitoa kikamilifu na kutoa mioyo yao nusu nusu ambayo huzuia kazi ya ukweli na kuleta giza katika kanisa la Mungu.
Hakuna njia yenye uhakika zaidi ya kutufanya tudhoofike katika mambo ya kiroho kama kuwa na wivu, hali ya kushuku, kujawa na kutafuta makosa na kupuuzia dhambi….Unapokuwa pamoja na watu wengine, linda maneno yako…. Kama kuipenda kweli kuko ndani ya moyo wako utaongea ile kweli. Utaongea juu ya tumaini lenye baraka ulilo nalo katika Yesu. Kama una upendo katika moyo wako utatafuta kumuimarisha na kumjenga ndugu yako katika imani iliyo takatifu zaidi. Kama neno litaponyoka katika midomo lenye kuharibu tabia ya rafiki au ndugu yako, usiendekeze uzungumzaji huo mbaya kwani hiyo ni kazi ya adui. Kwa upole mkumbushe mzungumzaji kwamba Neno la Mungu linakataa uzungumzaji wa namna hiyo. Tunapaswa kumimina kiini cha kila kitu ambacho kinalinajisi hekalu ya roho, ili Kristo aweze kukaa ndani. Mwokozi wetu ametuambia namna tunavyoweza kumfunua kwa ulimwengu. Kama tutadumisha Roho Wake, kama tutadhihirisha upendo Wake kwa wengine, kama tutalinda maslahi ya kila mmoja wetu, kama tutakuwa watu wema, wavumilivu, wastahimilivu, ulimwengu utakuwa na ushahidi wa matunda tutakayozaa kwamba sisi tu watoto wa Mungu. Ni umoja katika kanisa ambao huliwezesha kanisa kuufanyia kazi mvuto wenye ufahamu kwa waumini na wakazi wa dunia. Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi. Yohana 13:35.
Dini ya Kristo ni zaidi ya msamaha wa dhambi; humaanisha kwamba dhambi zimeondolewa na kwamba sehemu iliyobaki tupu imejazwa na Roho Mtakatifu. Inamaanisha kwamba akili hutiwa nuru ya mbinguni na moyo huondolewa ubinafsi wote na kujazwa na uwepo wa Kristo. Wakati hili linapofanyika kwa washiriki wa kanisa, kanisa litakuwa hai na lenye kufanya kazi. Tutakapoweka mioyo yetu katika umoja na Kristo na maisha yetu yakapatikana na kazi Yake, Roho ambaye alishuka wakati wa Pentekoste atamwagwa kwetu. Tutakuwa imara katika nguvu ya Kristo na kujazwa na ukamilifu wa Mungu……Tutajitoa kwa Kristo, na kuweka wakfu vyote tulivyo navyo, uwezo wetu wote katika huduma ya Kristo. Tutaitangaza imani yetu vyema, tutamtumikia Mungu kwa kuwahudumia wale wanaohitaji msaada wetu. Ndipo tutaruhusu nuru yetu kuangaza kwa matendo mema.
Kama wanafunzi wa Yesu walivyojazwa na nguvu ya Roho Mtakatifu, wakaenda kutangaza injili, hivyo hivyo watumishi wa Mungu wanatakiwa kwenda kutangaza injili. Kila ambaye anamulikiwa na nuru ya ukweli wa leo anapaswa kuamshwa kwa kuwahurumia wale walioko gizani. Kutoka kwa washiriki wote nuru yapaswa kuakisiwa katika mionzi iliyo wazi na ming’aavu. Kazi kama ile ile aliyoifanya Bwana kupitia kwa wajumbe wake baada ya siku ya Pentekoste anasubiri kuifanya hata leo. Katika kipindi hiki, wakati mwisho wa mambo yote umekaribia, ari ya kanisa yapaswa kuzidi ile ya kanisa la awali. Ari kwa ajili ya utukufu wa Mungu iliwafanya wanafunzi kubeba ushuhuda wa ukweli kwa nguvu nyingi. Je ari hii haipaswi kuichoma mioyo yetu kwa ajili ya kuwiwa kuhadithia kisa cha upendo uokoao wa Kristo aliyesulubishwa?

Maswali ya Kujitathmini:
1. Je wewe, mshiriki wa kanisa hai la Kristo, wawezaje kuhimiza umoja na upendo kwa ndugu zako?
2. Tafakari kwa maombi kama unahitaji kusamehe, au kuomba msamaha au kupatana na ye yote ndani au nje ya kanisa.

0 comments:

Post a Comment