Subscribe:

Wednesday, 13 January 2016



SIKU YA – 8:

     KRISTO AKIAKISIWA KATIKA FAMILIA:

“Wapenzi, na mpendane; kwa kuwa pendo latoka kwa Mungu, na kila apendaye amezaliwa na Mungu, naye anamjua Mungu.” 1Yohana 4:7

Mapendekezo ya Utaratibu wa Kipindi cha Maombi
Kusifu (takribani dakika 10)
Anzeni kipindi cha maombi kwa kumsifu Mungu kwa jinsi alivyo (Tabia Yake). Yeye ni mwenye neema n.k
Msifu Mungu kwamba Yeye ni Baba wa familia ya wanadamu duniani.
Msifu Mungu kwamba anataka familia ya kibinadamu iakisi uzuri Wake na tabia Yake.
Kuungama na Kudai Ushindi dhidi ya dhambi
Muombe Mungu akuonyeshe dhambi unazohitaji kuziungama kwa siri. Dai ushindi juu ya dhambi hizo.
Muombe Mungu msamaha kwa nyakati ambazo hukumuakisi Mungu katika familia yako.
Muombe Mungu msamaha kwa nyakati ambazo hukuwaheshimu na kuwatii wazazi wako pamoja na ndugu mliozaliwa nao.
Mshukuru Mungu kwamba anakusamehe kulingana na 1Yohana 1:9.
Sala na Maombezi
Muombe Mungu ajaze moyo wako kwa Roho Mtakatifu na kukufanya kuwa mfano hai kwa familia yako
Muombe Mungu ili kila mwanafamilia katika famila yako avutwe karibu na Kristo
Muombe Mungu azilinde familia za Kiadventista dhidi ya mashambulio ya Shetani, zikiwemo familia katika kanisa lako mahalia. Muombe Mungu kwa ajili ya uponyaji pale inapohitajika.
Omba ili kwamba viongozi wa kanisa (mchungaji wako wa mtaa, wachungaji wa konferensi, unioni, divisheni na Makao Makuu ya Kanisa) pamoja na familia zao wamuakisi Kristo kwa ulimwengu.
Omba kwa ajili ya mavuno ya pekee ya roho kutokana na mbegu zilizopandwa wakati wa mradi wa usambazaji wa kitabu cha Tumaini Kuu katika mifumo yake yote.
Omba kwamba wazazi wamuakisi Kristo kwa watoto wao na kuwalea kwa ajili ya Ufalme.
Omba ili kwamba Mungu alete uelewa kamili wa njia aliyoitumia Kristo (huduma kamili ya uponyaji) ili kwamba washiriki wote wasaidie watu kwa kuwapatia mahitaji yao na kufuata kilelezo cha Kristo katika kuhudumia wengine.
Omba kwa ajili ya muunganiko wa harakati za uinjilisti na ushuhudiaji wa kila mwanaume, mwanamke na watoto wote wa Kiadventista kote duniani. Omba kwamba tujazwe na Roho Mtakatifu tunapojisalimisha kwa uongozi wake katika maisha yetu.
Msihi Bwana kwa niaba ya familia za Kiadventista ili ziwe kielelezo cha jinsi Kristo anavyoweza kuleta amani na upendo majumbani, kuondoa kila unyanyasaji na misongo kupitia kwa nguvu itakasayo ya haki ya Kristo na kuelekeza watu kwa kuja kwa Kristo kuliko karibu na hatimae kuungana na familia ya milele ya Mungu huko mbinguni.
Utume katika Miji Mikuu Omba kwa ajili ya Divisheni ya Euro-Asia na miji wanayoifanyia kazi: Moscow, Kiev, Kishinev, Donetsk, Kharkov, Minsk, St. Petersburg, Novosibirsk, Krasnoyarsk, Khabarovsk, Rostov -on-Don, Tbilisi, Yerevan na Almaty. Omba kwa ajili ya maelfu ya huduma za kuwafikia watu na matukio yanayoendelea ya uvunaji wa roho.
Omba ili kwamba watu saba au zaidi katika orodha yako waone hitaji lao na kufungua mioyo yao kwa Roho Mtakatifu.
Omba kwa ajili ya mahitaji binafsi uliyo nayo.
Shukrani (dakika 10)
Mshukuru Mungu kwamba anafanyia kazi mioyo ya wanafamilia wako.
Mshukuru Mungu kwamba yu tayari kukusafisha, kukutakasa na kukaa ndani yako na ndani ya familia yako.
Mshukuru Mungu kwamba Yesu ametupatia kielelezo cha jinsi ya kuwaheshimu wazazi wetu pamoja na kuwapenda ndugu tuliozaliwa nao.
Mapendekezo ya Nyimbo
Kuwa na Yesu Nyumbani no. 204, Panapo Pendo no.184, Upendo ni Furaha no. 199

 KRISTO AKIAKISIWA KATIKA FAMILIA:

“Wapenzi, na mpendane; kwa kuwa pendo latoka kwa Mungu, na kila apendaye amezaliwa na Mungu, naye anamjua Mungu.” 1Yohana 4:7
Dini ya Kristo itatuongoza katika kufanya mambo yote mema kadiri iwezekanavyo, kwa watu wa daraja la juu na la chini, kwa matajiri na maskini, kwa wenye furaha na wale wanaoonewa. Lakini haswa itatuongoza katika udhihirisho wa wema katika familia zetu wenyewe. Dini hiyo itadhihirika katika matendo ya adabu, na upendo kwa baba, mama, mke na mtoto. Tunapaswa tumwangalie Yesu, kukamata roho Yake, kuishi katika nuru ya wema Wake na upendo na kuakisi utukufu Wake kwa wengine.
“Basi mtiini Mungu, Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.” Yakobo 4:7
Kama utajitoa kikamilifu kwa Yesu, ataumba ndani yako tamanio la kina kwa ajili ya urafiki na Mungu, nawe utajazwa shauku ya kuakisi wema Wake na upendo Wake katika maisha yako na tabia yako kwa familia yako na kwa wale wasioufahamu upendo Wake. Kwa kupanda uvumilivu, upole, ustahimilivu, kwa kuonyesha heshima na kuwapa utii mama yako na baba yako kama impendezavyo Bwana, utakuwa ukitoa ushuhuda katika maisha yako ya kila siku kwamba ukweli una nguvu ya kutakasa tabia.
Ni swala gumu kurekebisha mambo magumu katika familia, hata pale ambapo mume na mke wanatafuta kufanya hivyo kama wameshindwa kusalimisha mioyo yao kwa Mungu.
Aniaminiye mimi, kama vile maandiko yalivyonena, mito ya maji yaliyo hai itatoka ndani yake. Yohana 7:38.
Kama mapenzi ya Mungu yatatimizwa, mume na mke wataheshimiana na kuotesha upendo na ujasiri. Cho chote kile ambacho chaweza kuharibu amani na umoja wa familia chapaswa kuzuiwa kwa uthabiti na utu wema pamoja na upendo vyapaswa kudumishwa. Mtu yule ambaye anadhihirisha roho ya upole, ustahimilivu na upendo atagundua kuwa roho ile ile itaakisiwa toka kwake. Mahali ambapo Roho wa Mungu anatawala, hakutakuwa na maongezi yasiyofaa katika mahusiano ya ndoa. Kama kweli Kristo atajengwa ndani kwa kina, tumaini la utukufu, kutakuwa na umoja na upendo nyumbani. Kristo akikaa katika moyo wa mke kutakuwa na makubaliano pamoja na Kristo anayekaa ndani ya moyo wa mume. Watafanya bidii pamoja kwa ajili ya kwenda katika makao ambayo Kristo amekwenda kuandaa kwa wale wampendao.
Lazima tuwe na Roho wa Mungu, au kamwe hatutakuwa na mwafaka nyumbani. Mke, kama ana roho wa Kristo atakuwa makini na maneno yake, atajizuia, atakuwa mtii na bado hatajisikia kana kwamba ni mtumwa, lakini mwenzi wa mumewe. Kama mume ni mtumishi wa Mungu, hatamtawala mke wake, hatakuwa dikteta na mkali. Hatutaweza kudumisha upendo nyumbani kwa kuwa waangalifu kupita kiasi, kwani Roho wa Bwana akiwepo nyumbani, panakuwa sehemu ya mbinguni……mmoja anapokosea, mwingine atafanyia mazoezi ustahimilivu kama wa Kristo badala ya kumpa kisogo mwenzake na kuondoka.
Kama unayo matazamio makubwa na kusudi la kufika katika kiwango cha juu, maisha ya nyumbani yanaweza kukupa adabu bora zaidi. Kama ukikosea nyumbani, utakosa katika kila lengo na kila jitihada. Anza nyumbani ili kukamilisha tabia ambayo Mungu ataikubali, tabia itakayofanya uwe mbaraka nyumbani, na utakapokuwa mbali na nyumbani, hautashindwa kuwa mbaraka kwa wale utakaokutana nao. Dini inayofanyiwa mazoezi nyumbani huakisi mbali zaidi ya wigo wa hapo nyumbani.

Maswali ya Kujitathmini:
1.Je unawezaje kuongoza familia yako kwa kielelezo cha maisha tele kwa Kristo?
2.Je daima umekuwa mwanafamilia mzuri? Je kuna mambo ambayo unahitaji kurekebisha? Je wahitaji kuifanya familia yako kuwa kipaumbele zaidi ya mambo mengine?

0 comments:

Post a Comment