Subscribe:

Wednesday, 13 January 2016



SIKU YA – 5:

ZAIDI YA KUSHINDA:

“Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda.” Wakorintho 8:37.

Kusifu (takribani dakika 10) Anzeni kipindi cha maombi kwa kumsifu Mungu kwa jinsi alivyo yaani tabia Yake. Msifuni kwa uaminifu Wake na kwamba Yeye ni kimbilio. Msifu Mungu kwamba yote unayotakiwa kufanya ni kukaa ndani ya Kristo ili upate ushindi dhidi ya dhambi. Msifu Mungu kwamba Yesu alipata ushindi dhidi ya dhambi pale msalabani. Kuungama na Kudai Ushindi dhidi ya Dhambi (dk5) Muombe Mungu akuonyeshe dhambi ambazo unahitaji kuziungama kwa uwazi na zile ambazo unahitaji kuziungama faraghani. Dai ushindi dhidi ya dhambi hizo. Je kumekuwepo na nyakati ambazo hukujisikia kwamba ulitaka kuishinda dhambi? Muombe Mungu msamaha. Muombe Mungu aweke tamanio ndani ya moyo wako la kuishinda dhambi. Muombe Mungu msamaha kwamba sisi, kama kanisa bado hatujaweza kuishinda dhambi. Mshukuru Mungu kwamba anakusamehe kulingana na 1 Yohana 1:9. Sala na Maombezi (dakika 35) Omba kwamba Mungu akupe tamanio la kuishinda dhambi. Ombea wanafamilia na marafiki ambao pia wanahitaji kupata ushindi dhidi ya dhambi. Ombea mahali ambapo katika maisha yako bado unahitaji kupata ushindi dhidi ya dhambi. Muombe Mungu akupe ushindi kamili. Muombe Mungu akusaidie uamini kwamba Yeye anaweza kukupatia ushindi kamili dhidi ya dhambi. Je bado unashikilia sanamu katika maisha yako? Zilete sanamu hizo mbele za Mungu na muombe akupe chuki moyoni mwako dhidhi ya sanamu hizo.
Omba ili viongozi wa kanisa (Mchungaiji wako wa mtaa, wachungaji wa konferensi, unioni, divisheni na Makao Makuu ya Kanisa) wamruhusu Mungu awape ushindi dhidi ya dhambi.
Omba ili Mungu akufanye uwe mnyenyekevu ili uweze kuona udhaifu wako na kuomba nguvu ya kushicnda udhaifu huo.
Omba kwa ajili ya mipango mikubwa ya uinjilisti na huduma nje ya kanisa katika divisheni zote 13 pamoja na unioni moja iliyo pamoja na divisheni hizo, unioni ya (Middle East and North Africa Union).
Omba kwa ajili ya mafanikio katika “Utume Katika Majiji” na katika kufikia maeneo ya vijijini. Utume katika Miji Mikubwa –
 Omba kwa ajili ya divisheni ya South America na miji 74 ambayo wameichagua ili kuihudumia. Omba pia kwa ajili ya Divisheni ya Pasifiki ya Kusini na miji ambayo wameichagua kuifikia kwa ajili Kristo: miji hiyo ni Sydney, Christchurch, Lae, Apia.
 Omba ili kwamba Mungu atume watenda kazi na aweze kubariki jitihada zao.
 Omba ili Mungu aendelee kuongoza kanisa Lake na kuwapa washiriki ushindi dhidi ya dhambi. Omba ili watu saba (au zaidi) katika orodha yako waweze kuona hitaji lao na kufungua mioyo yao kwa Roho Mtakatifu.
Omba kwa ajili ya mahitaji yako binafsi uliyo nayo (Mithali 3:5, 6).
Shukrani (takribani dakika 10) Mshukuru Mungu kwamba yupo radhi kukupatia haki Yake. Mshukuru Mungu kwamba Yeye ndiye “Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema.” Wafilipi 2:13 Mshukuru Mungu kwa ajili ya maisha ya Yesu yasiyo na dhambi na jinsi ambavyo ametuonyesha jinsi ya kuwa washindi. Mshukuru Mungu kwamba anajibu maombi uliyoomba kulingana na mapenzi Yake.
Mapendekezo ya Nyimbo: Si Mimi Kristo no. 17, Usinipite Mwokozi no.22, Mtazame Mwokozi no.212, Mwamba Wenye Imara no. 192

ZAIDI YA KUSHINDA.

“Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda.” Wakorintho 8:37
Katika pambano lao na Shetani, familia ya kibinadamu inao msaada wote aliokuwa nao Kristo. Hawatakiwi kushindwa. Wanaweza kuwa zaidi ya washindi kupitia Yeye ambaye aliwapenda na akatoa maisha Yake kwa ajili yao….Mwana wa Mungu katika ubinadamu Wake alipambana na hali mbaya vivyo hivyo, majaribu mazito ambayo hutushambulia – majaribu ya uchu wa chakula, kuwa na kiburi kuthubutu kuenenda mahali ambapo Mungu hajaongoza na kuelekea katika kumuabudu mungu wa ulimwengu huu, kutoa mhanga umilele wa mbinguni kwa anasa zinazovutia za ulimwengu huu. Kila mmoja atajaribiwa, lakini Neno linasema kwamba hatutajiribiwa kupita tuwezavyo kuvumilia. Tunaweza hata hivyo kukataa na kumshinda adui mwenye hila. Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili. (1Wakorintho 10:13)
Kazi yetu ya katika maisha tuliyopewa ni kazi ya maandalizi ya maisha ya umilele, na tutakapokamilisha kazi hii kama Mungu alivyowezesha tuifanye, kila jaribu litakuwa kwa kutufanya tusonge mbele; kwani tutakapokataa kuhadaika na jaribu hilo tutasonga mbele katika maisha ya kimbingu. Katika joto la pambano, wakati tunapojihusisha kikamilifu katika vita ya kiroho, mawakala wasioonekana kwa macho wako kando yetu, waliokabidhiwa mamlaka na mbingu kutuongoza katika mapambano yetu na wakati wa hatari, tunapatiwa nguvu, uthabiti na uwezo, na tunakuwa na nguvu zaidi ya ile ya kibinadamu.Lakini isipokuwa pale tu wakala wa kibinadamu ataweka nia yake kupatana na ile nia ya Mungu, hadi atakapokuwa ameachana na sanamu na kushinda kila mazoea mabaya, kamwe hatafanikiwa katika pambano ila hatimaye atashindwa. Wale ambao watakuwa washindi lazima waingie katika pambano pamoja na wakala wasioonekana, ufisadi ulio ndani ya moyo wapaswa kushindwa, na mawazo yote yapaswa kutiishwa kwa Kristo na kusalimishwa kwa Kristo. Roho Mtakatifu daima yuko kazini akitafuta kutakasa, kusafisha na kuadibisha roho za wanadamu ili kwamba wafae katika jamii ya watakatifu na malaika na kama washindi waweze kuimba wimbo wa ukombozi, wakirudisha utukufu na heshima kwa Mungu na kwa Mwanakondoo katika nyua za mbinguni.. Hatuna adui wa nje ambaye tunaweza kumuogopa. Pambano letu kuu liko katika ubinafsi ambao haujawekwa wakfu, Tutakapoishinda nafsi, tutakuwa zaidi ya washindi kupitia Yeye ambaye alitupenda. Ndugu zangu, kuna uzima wa milele tunaohitaji kuupata. Hebu tupige vita vizuri vya imani. Wakati tulio nao si ujao, lakini sasa.
Lakini msisahau kutenda mema na kushirikiana; maana sadaka kama hizi ndizo zimpendezazo Mungu, (Waebrania 13:16)
Kuishi maisha aliyoishi Mwokozi, kushinda kila shauku yenye ubinafsi, kutimiza wajibu wetu kwa Mungu na kwa wenzetu kwa ujasiri na kwa moyo uliochangamka hutufanya tuwe zaidi ya washindi. Hii hutuandaa kusimama mbele ya kiti kikuu cheupe cha enzi bila mawaa wala makunyazi, tukiwa tumesafisha mavazi yetu ya tabia na kuyasafisha kuwa meupe katika damu ya Mwanakondoo. Nguvu inayotawala watu ya uchu wa chakula itaongoza maelfu kupotea, wakati ambapo kama wangeshinda katika jambo hili, wangekuwa na nguvu ya kimaadili kuwasaidia kupata ushindi juu ya majaribu yote ya shetani. Lakini wale ambao ni watumwa wa uchu wa chakula watashindwa kukamilisha tabia ya Kikristo. Uasi unaoendelea wa mwanadamu kwa miaka elfu sita umeleta matunda ya magonjwa, maumivu na kifo. Tunapokaribia mwisho wa wakati, majaribu ya shetani katika kuendekeza uchu wa chakula yatakuwa yenye nguvu zaidi na magumu kuyashinda.
Ndugu zangu, hebu tuweke yote hayo pembeni, hatuna haki ya kuelekeza mawazo yetu kwetu wenyewe, wala katika vipaumbele vyetu na yote yanayotupendeza. Hatupaswi kutafuta kudumisha kutambulika kwetu kwa namna iliyo ya pekee, wasifu wetu, au ubinafsi wetu, ambao utatutenganisha na watenda kazi wenzetu. Tuna tabia ambayo twapaswa kuidumisha lakini hiyo ni tabia ya Kristo. Tunapokuwa na tabia ya Kristo, tutaweza kuifanya kazi ya Mungu pamoja. Kristo aliye ndani yetu atakutana na Kristo aliye ndani ya wenzetu na Roho Mtakatifu ataleta muunganiko wa mioyo na matendo ambayo yatashuhudia kwa ulimwengu kwamba sisi ni watoto wa Mungu. Hebu Mungu atusaidie kuifia nafsi na kuzaliwa upya, ili Kristo aweze kuishi ndani yetu, kwa kanuni iliyo hai na itendayo kazi, nguvu ambayo itatufanya kudumu kuwa watakatifu.

Maswali ya Kujitathmini:
1. Je ni mapambano gani yaliyo makuu katika maisha yako? Je ni katika mambo gani unahitaji ushindi?
2. Je ni mambo gani yanayokuzuia kutokuwa zaidi ya mshindi? Salimisha mambo hayo kwa Mungu.

0 comments:

Post a Comment