Mnamo Mwaka 1904 wamishionari wa kwanza walifika Tanganyika wakitumwa na
Konferensi ya Ujerumani kwa ajili ya kazi ya injili. Walifika Dar es
Salaam mwezi wa Disemba na kuelekea milima ya Upare iliyoko Kaskazini
Mashariki mwa Tanzania. Walifanikiwa kuanzisha kituo cha misheni katika
bonde la Giti. Tangu Mwaka 1905 – 1912 vituo vya Kihurio, Suji na Gunta
viliweza kuanzishwa ambapo waumini wa kwanza walikuwa wanane tu.
Mpaka
kufikia mwaka 1950 injili ilikuwa imeenea maeneo mengi tofauti tofauti
hapa nchini na Mwaka 1960 Makao Makuu ya Kanisa yalianzishwa huko
Busegwe mkoani Mara na baadae kuhamishiwa Arusha eneo la Njiro kama
Tanzania Union.
Mnamo
mwaka 2013 tarehe 4 Disemba iliyokuwa Tanzania Union ilitangazwa rasmi
na mwenyekiti wa Kanisa la Waadventista wa Sabato Kanda ya Afrika
Mashariki na Kati Mchungaji Blassious Ruguri kuwa na Union mbili ambazo
ni Union Konferensi ya Kaskazini mwa Tanzania na Union Mision ya Kusini
mwa Tanzania. Union Konferensi ya Kaskazini mwa Tanzania inajumuisha
mikoa 13 ambayo ni Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga, Singida, Simiyu,
Shyinyanga, Mara, Mwanza, Tabora, Kigoma, kagera na Geita. Union hii
ina idadi ya makanisa 1929 yenye jumla ya washiriki 404,159.
Union
Conference ya Kaskazini mwa Tanzania ina majimbo madogo 4, ambayo ni
Mara Conference, South Nyanza Conference (SNC), West Tanzania Conference
(WTC) na North East Tanzania Conference (NETC). Jimbo la NETC
linajumuisha mikoa 4 ambayo ni Tanga, Kilimanjaro, Manyara na Arusha
lenye jumla ya washiriki washiriki 67,216. Kanisa la Waadventista wa
Sabato Burka linapatikana ndani ya Jimbo la Kaskazini Mashariki mwa
Tanzania.
INJILI ARUSHA
Mnamo mwaka 1954 Eliamani Manase aliyekuwa
muumini wa Kanisa la Waadventista wa Sabato alihamia katika Mkoa huu
kikazi na ndiye aliyeanzisha injili katika Mkoa huu wa Arusha. Kwa
juhudi zake binafsi alitafuta waumini wenzake wa kanisa hili na
alifanikiwa kuwapata wachache ambapo walianzisha kundi la shule ya
Sabato. Walikutana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukosa
sehemu ya kuabudia, lakini Bwana ni Mwema kwani ilipofika mwaka 1961
walifanikiwa kupata eneo huko Sanawari wakiwa waumini 4 na wanafunzi 2.
Baadae walipata eneo lingine huko Meru kwa mzee Ndelekwa Ikamba ambapo
namba ya waumini iliendelea kuongezeka na kufikia watu 7.
Mwaka
1962 familia ya Mama Yunis Natogolwa Kuga walihamia Arusha na bado
hapakuwa na kanisa isipokuwa tawi hilo moja la Shule ya sabato.
Washiriki hawa walifanya kazi ya uinjilisti katika mazingira magumu
kwani kulikuwa na kanisa moja tu na watu walikuwa wakitembea mwendo
mrefu kwenda kanisani lakini pia kutawanya vijizuu na masomo ya Sauti ya
Unabii. Katika mwaka huo waliendesha effort ya kwanza ya nyumba kwa
nyumba iliyoendeshwa na Mchungaji Bender maeneo ya Sanawari na watu
wasiopungua 10 walibatizwa.
BURKA KUPATIKANA
Mnamo
mwaka 1967 jengo la kanisa la Burka lilinunuliwa toka kwa makaburu wa
Afrika ya Kusini. Washiriki wakiwa na mchungaji Bender walifurahi sana
na kumshukuru Mungu kwa kupata nyumba ya ibada. Waliendelea kufanya kazi
ya uinjilisti kwa bidii japo katika mazingira magumu kwani walikuwa
wakitembea kwa miguu mwendo mrefu lakini Bwana aliwawezesha na idadi ya
waumini iliongezeka.
Sabato ya kwanza kusali katika kanisa hili
alieongoza ibada alikuwa Mchungaji Cril Bender na Mashemasi walikuwa
Upendo Yoel, Yunis Natogolwa Kuga, William Senkoro na Eliamani Manase,
Mtunza Kanisa wa kwanza alikuwa Mbonea Kiondo ambaye pia alikuwa Mkuu wa
Kundi hilo la Burka. Mwinjilisti wa kwanza wa Vitabu alikuwa ni
Elibariki Misheto aliyetumwa kutoka Field. Mwaka 1964 familia ya John
Mhina iliongezeka.
Siku za pasaka walikuwa wakisali huko Majengo
Moshi na hiyo ilikuwa kila Sabato ya kwanza ya kila Mwezi. Mwaka 1965
Ubatizo ulifanyika na aliyebatiza alikuwa Mchungaji Yohana Lusingu,
waumini waliobatizwa ni familia ya Mzee Ndelekwa, Upendo Yoel, Jotham
Lukwaro na Daud Obayo.
Mwaka 1966 ulifanyika mkutano mkubwa kwa miezi
sita, mikutano hiyo ilifanyika katika eneo la Hosptali ya Kaloleni.
Waliobatizwa katika mkutano huo ni: Nairoki Lotanywaki na kijana wake
Nsinyari na binti zake wawili. Mchungaji wa kwanza alikuwa Tumaini
Abraham ambaye alikufa kwa kuumwa na nyuki, baadae alifuata Mchungaji
Uze Kajiru baada ya Mtumishi wa Bwana kulala mauti.
Makundi ya kwanza
kutoka Burka yalikuwa ni: Tengeru, Monduli, Kijenge likifuatiwa na
kundi lililokuwa likisali katika Shule ya Msingi Meru, Kundi la Unga
Limited lilikuwa likisali katika Shule ya Msingi Sinoni. Mtaa wa kwanza
kutengwa toka Burka ulikuwa ni Mtaa wa Meru ikifuatiwa na Mtaa wa Njiro
na Sanawari.
Kanisa hili limechungwa na Wachungaji wafuatao:
Mch. Tumaini Abraham
Mch. Uze Kajiru
Mch. Daniel Nahato
Mch. Anderson Fue
Mch. Joseph Namfua
Mch. Samwel Panga
Mch. Elisante Mkiramwene
Mch. Elias Peter Lomai
Mch.John Wilfred Kimbute
Mch. Isaya Kanana
Kwa
sasa Kanisa hili linachungwa na Mchungaji Simon Mnyindo akisaidiana na
Wazee wa Kanisa Zephania Malima, Daud Charles, Steven Katengu na Elia
Nyeura. Mashemasi ni Bennett Msovu na Catherine Buyabara pamoja na
Wahazini Simeon Matiko, Helen Mong’ateko na Sitty Gamba.
Kanisa hili
linayo kwaya ya Kanisa iliyosajiliwa rasmi mwaka1986 ikiwa na wanakwaya
40 chini ya mwenyekiti na Mwalimu Lazaro Jonas akisaidiana na waalimu
Joshua Otuoro na Malaki Saka (ambaye kwa sasa ni Marehemu).
Mpaka
sasa Kwaya imefanikiwa kutoa matoleo 24 ya Audio na 4 ya DVD. Kwaya hii
kwa kwa mwaka huu wa 2016 imefanikiwa kusajili wanakwaya wapatao 80 na
walimu ni Aloyce Mabula, Zadock Otieno, Joshua Otuoro, Samwel Ongiri,
jerry Kairanya na Lameck Chacha.
Kwa neema ya Bwana Kanisa la Burka
limeendelea kufanya kazi ya utume kwa bidii na limefanikiwa kuongeza
idadi kubwa ya washiriki na hivyo kuweza kuwa na mitaa 12 na makanisa
takriban 50 yenye jumla ya washiriki 20,013 kati ya hao washiriki 736
wanatoka kanisa la Burka. Kanisa pia limefanikiwa kupeleka injili maeneo
ya umasaini na kuweza kujenga makanisa maeneo ya Lovilukunyi,
Ngaramtoni ya Chini, Olchorovus, Matevesi na Engorora. Kanisa pia
limefanikiwa kununua vyombo vya sauti.
Kwa sababu idadi ya washiriki
inaongezeka Kanisa linao mpango wa muda mrefu kuwa na Jengo kubwa la
ibada ili kuikidhi mahitaji ya kanisa. Lakini pia kuna mpango wa muda
mrefu wa kuwa na kituo cha mvuto (Center of Influence) Pamoja na nyumba
ya Mchungaji. Kanisa limeanza mpango huo wa ujenzi na washiriki
wameshirikishwa kwa kuanza kuchangia vifaa mbalimbali vya ujenzi.
MOTTO: BURKA 2016 - ONDOKA UANGAZE, YESU ANAKUJA